Katika kuttekeleza
sera ya Chama Cha Mapinduzi, Mkuu wa wilaya ya Hanang
Mh. Christina Mndeme, aliwakutanisha vijana kutoka kata zote za
wilaya ya Hanang, na baada ya kujadili changamoto za kimaisha zinazowakabili vijana
hao kwa pamoja walikubaliana kuanzisha SACCOS ambayo itakuwa chombo cha
kuwaunganisha vijana hao na kutoa mikopo yenye masharti nafuu, itakayowawezesha
vijana hao kujikomboa kiuchumi.
Mkuu wa wilaya ya Hanang Mhe. Christina Mndeme. |
Akizungumza na gazeti hili mkuu wa wilaya ya
Hanang alisema “Shirika
hili lilianzishwa kwa lengo la kuwakwamua vijana kichumi na kupanua wigo wa
ajira kwa vijana na kuamsha vipaji na
uwezo wao wa kufanya kazi kwa kuunda vikundi vidogovidogo vya wajasiriamali na
kuwapa elimu na mikopo yenye masharti nafuu itakayowawezesha vijana kujipatia
kipato na kuwa chachu ya maendeleo yao, jamii inayowazunguka na Wilaya kwa
ujumla”
Akitolea ufafanuzi mkuu wa wilaya ya Hanang
alisema wameanzisha vikundi vitano ambavyo ni kikundi cha wafuga nyuki,
waendesha bodaboda, kilimo, wafugaji wa kuku wa kienyeji na kikundi cha
wafyatua matofali ya kisasa kwa technolojia ya hydroform,
Akaindelea
kufafanua mkuu wa wilaya ya Hanang alisema “Shirika
hili lilianzishwa chini ya sheria ya vyama vya ushirika na 20 ya mwaka 2003, na
kanuni za vyama vya ushirika za mwaka 2004, na kusajiliwa tarehe 04/12/2013 kwa
nambari ya usajili MNR/144 Ikiwa na wanachama waanzilishi 316, na sasa
tunajivunia kuwa na wanachama hai zaidi ya 400 na bado tunawahamasisha wote wa
kike na wa kiume waishio wilaya ya Hanang wenye umri kati ya miaka 15 na 35
wajiunge na Saccos hii”
Aidha mwenyekiti wa kamati ya mpito ya SACCOS
hiyo Bw. Dominick Duncan alisema
kuwa “Hii inaonesha nia ya dhati
ya serikali katika kutokomeza umasikini, na kuwakomboa vijana ambao ndio nguvu
kazi ya taifa” akaongeza “Vijana wengi tulikuwa hatuna ajira rasmi, hivyo
hatukuwa na kipato cha uhakika, hii ilitupelekea vijana wengi kukosa matumaini
na kujiona kama kundi lililosahaulika katika jamii, lakini SACCOS hii imefufua
matumaini yetu, na leo najivunia kuwa kijana wa kitanzania”